Sunday, July 10, 2011

Bob Rudala awa bosi wa bendi ya Kalunde

Mwimbaji wa siku nyingi wa muziki wa dansi, Bob Rudala, aliyejiunga na bendi ya Kalunde hivi karibuni akitokea katika bendi ya InAfrika, ameteuliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo.
Kwa mujibu wa Meneja wa bendi hiyo, Doborah Nyangi, uongozi wa juu ndio umemteua Rudala kushika nafasi hiyo ambayo awali ilikuwa ikikaimiwa na mwimbaji Junior Grengo.
Deborah alisema, Rudala aliteuliwa kuwa kiongozi wa bendi hiyo tangu wiki iliyopita baada ya uongozi wa juu wa Kalunde kukutana na kuamua kwamba ndiye apewe jukumu la kuiongoza bendi.
"Tunaamini kwamba ana uwezo mkubwa wa kuongoza, ndio maana mabosi wetu wamekaa na kuamua kumteuwa kuwa kiongozi wa bendi yetu kwani ni mwanamuziki mzoefu ambaye amefanya hii kwa muda mrefu," alisema Deborah.
Alifafanua kwa muda mrefu bendi hiyo haikuwa na kiongozi ambapo Junior Grengo alikuwa akiishikilia kwa muda ambapo sasa nafasi hiyo amepewa Rudala huku Deo Mwanambilimbi akiendelea kuwa rais wa bendi.
Aidha, alisema kuwa Rudala amechukuwa nafasi ya uongozi wa bendi wakati ikiendelea na mazoezi ya kuandaa nyimbo za albamu ya pili ikiwa imekamilisha nne za 'Masumbuko', 'Sisee' na 'Fungua' na 'Ulinipendea Nini'.
"Tunafanya mazoezi ya kuandaa nyimbo za albamu ya pili huku tufanya maonyesho kama kawaida kwa siku za Jumatano na Ijumaa ambapo huwa tunatoa burudani katika ukumbi wa Triniti uliopo Oysterbay," alisema.
Meneja huyo aliongeza kuwa siku ya Jumamosi Kalunde imekuwa ikitoa burudani katika ukumbi wa Joevic Mbezi Beach na kisha Jumapili huwa ndani ya ukumbi wa Giraffe Hotel ambao pia upo Mbezi Beach.
Wakati huo huo Meneja hjuyo alisema, bendi hiyo inayotumia mtindo wa 'Lekendepuke', inajivunia wanenguaji wake wawili, Queen Vero na Aminatha Othman, kwa madai kwamba wanajua kazi na wanajituma vilivyo wawapo jukwaani.
Hata hivyo, alibainisha kuwa wingi wa wanenguaji kwenye bendi kama yao haina umuhimu wowote hasa kwa kuzingatia kwamba huwa inapiga muziki kwenye kumbi tulivu ambazo hazihjitaji kuwa na kundi kubwa la wanenguaji.

No comments:

Post a Comment