Wednesday, July 6, 2011

Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere aja na mbinu za kuboresha elimu jimboni mwake

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara, Vicent Nyerere (Chadema), amesema kuwa anajiandaa kujenga maabara ya kisasa itakayotumiwa na shule tano za sekondari za kata zilizojengwa kwenye kata moja.
Nyerere ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Jimbo, alisema hayo alipokuwa akizungumzia mkakati wa kuboresha elimu kwenye jimbo lake.
"Uchache wa maeneo ya kujenga shule, ilibidi shule za sekondari za Bweri, Nyabisarye, Iringo, Nyamatare na Kamunyonge zijengwe kwenye kata moja ya Bweri," Nyerere.
Mbunge huyo alisema kuwa kwa hali hiyo inabidi ijengwe maabara moja kubwa na ya kisasa kwenye shule ya sekondari ya Bweri ambayo itakuwa inatumiwa na wanafunzi wa shule hizo tano.
Alisema maabara hiyo itajengwa kwa fedha za mfuko wa jimbo ambapo aliongeza kuwa hadi sasa mfuko huo una  shilingi milioni 17 na kwamba ana uhakika kwa ushirikiano na Manispaa mkakati huo utafanikiwa.
Alifafanua kuwa anaendelea kuwasiliana na wataalam wakiwemo wahandishi wa Manispaa ya Mji wa Musoma kuona uwezekano wa kuangalia eneo na kisha kuandaa michoro ya jengo la maabara hiyo.
"Hiin pia haizuii kila shule kuwa na maabara yake ila nitakachokufanya ni kujenga maabara kubwa ambayo itakuwa na vifaa vyote kwa manufaa ya wanafunzi wa shule hizo tano zilizongwa kwenye kata moja," alisema.
Alisema, atafanya kila liwezekanalo kwa kushirikiana na viongozi wa Manispaa ya Mji wa Musoma ili kuhakikisha kwamba kwa mwaka mmoja ama miwili maabara iwe imekamilika na kuanza kazi.
"Nimesema tutajenga maabara ya kisasa nikiwa na maana itakuwa pia na chumba cha kompyuta zilizounganishwa na mtandao ili kuwasaidia wanafunzi kupata masomo kirahisi kwa njia ya mtandao," alisema.
Mbali na hilo, mbunge huyo alibainisha kuwa ubora wa maabara hiyo pia utaongezewa sehemu ambayo itatumika kufugia wanyama wadogo wakiwemo vyura na panya kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Aidha, aliwaomba wadau wa elimu wamuunge mkono katika juhudi zake hizo za kuboresha elimu jimboni mwake na hasa kampuni ya simu kutoa modem ili kupata mtandao mara baada ya maabara hiyo kuanza kazi.
"Moja vipaumbele vyangu wakati wa kampeni ilikuwa ni kuboresha elimu, hivyo ninaanzia kwenye maabara na kisha yatafuata maeneo mengine kulingana mfuko wa jimbo utakavyoruhusu," alisema.

No comments:

Post a Comment